blogu imeandikwa na Gastor Mapunda na Hannah Gibson
Mradi wa ‘Kuwaleta ndani walio nje’ ulianza mwaka jana, yaani 2019. Timu ya Mradi ilifanya warsha yake ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Zambia (maarufu kama UNZA) mjini Lusaka, Zambia. Hii ilikuwa mara ya kwanza timu yote kuweza kuona ana kwa ana, na pia kuweza kufahamiana. Ingawa sisi wawili tumeshafanya kazi pamoja nchini Tanzania na Uingereza. Kwa ujumla wake, ilikuwa ni fursa murua kufahamiana na wenzetu wa Botswana, Zambia na Uingereza.
Katika warsha hii ya kwanza tulizumgumza kuhusu hali za nchi zetu na miradi mbalimbali ya kuangalia lugha. Kwa mfano, tulifahamu kwamba katika nchi ya Tanzania, Kiswahili ni lugha rasmi pekee, ingawaje na Kiingereza pia kinatumika kwa kiasi fulani. Watoto wa chekechea na wa shule za msinigi wanafundishwa kwa lugha ya Kiswahili. Kwa wengi hii haileti shida kwa sababu wameshazoea kuongea Kiswahili nyumbani. Hata hivyo, nchini Tanzania kuna lugha nyingi. Na kutokana na hali hiyo, kuna baadhi ya maeneo ya Tanzania ambako lugha ya Kiswahili ni ngeni kwa baadhi ya wanafunzi. Hali hii ilitulazimu tuone namna ya kuweza kushiriki kutoa mchango wetu kwa kufanya utafiti katika baadhi ya maeneo hayo.
Pia, kuna shida nyingine inayohusiana na lugha ya kufundishia na kujifunzia wakati wa kuendelea na masomo na kufikia hatua ya elimu ya sekondari. Hapo lugha ya kufundisha ni Kiingereza, ingawa asilimia kubwa ya wanafunzi wametoka wa shule za msingi wakiwa wamejifunza kwa lugha ya Kiswahili. Hivyo, ni wanafunzi wachache tu waliopata fursa ya kusoma katika shule binafsi ndiyo walioweza kupata elimu yao kwa lugha ya Kiingereza, wengi wanaohudhria shule za serikali hawapati nafasi kujifunze Kiingereza kabla ya kufika shule ya sekondari. Hali hii ya mkanganyiko katika lugha ya kufundishia ni kikwazo kikubwa kwa wanafunzi wengi, na kwa walio wengi lugha imekuwa ni shida kubwa katika jitihada zao za kupata elimu bora. Kwa ujumla, hali inaathiri kwa kiasi kikubwa wanafunzi wengi kimasomo and inaleta ugumu katika kupata elimu.
Utafiti wetu unaangalia namna ambavyo wanafunzi na walimu wanapoteza wakati wa kujifunza umahiri mahsusi darasani kwa kujifunza lugha mpya – kwa wanafunzi wengi wa vijiji vya pembezoni, moja lugha hizo mpya ni Kiswahili, na kwa wale wanaoanza elimu ya sekondari lugha mypa ya pili ni Kiingereza. Tumefurahi sana kwa sababu tumeweza kutembelea shule mbalimbali vijijini na kuzumgumza na watato, walimu na wazazi pia. Tumeanza kupata picha ya hali ya elimu, hasa kuhusiana na muktadha wa lugha na elimu. Tumeshaanza na utafiti kwa njia za mahojiano katika maeneo ya Songea na Tabora, na pia kwa kuingia darasani na kuangalia michakato ya ufundishaji na ujifunzaji, na pia kwa kuwapa majaribio ya kusoma watoto wa shule za msingi katika maeneo hayo. Baada ya hapo, tutapata picha bayana ya uhusiano baina ya lugha za nje ya shule, yaani lugha za nyumbani/lugha za jamii kwa upande mmoja, na lugha ya ndani ya shule na darasani, yaani lugha rasmi ya Kiswahili, kwa upande mwingine.
Tuna matumaini makubwa kuwa utafiti wetu utaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha elimu na maendeleo kwa ujumla.